Majimbo Ataka Wageni Waheshimiwe na Uchunguzi Ufanywe Kwa Dhulma Wanayofanyiwa Wageni
Claire Nyako9 Sept 2026 5 min read
Share
Mbunge wa Kabuchai na mwanachama wa Bunge la Afrika, Majimbo Kalasinga, amelaani mazingira yanayowalazimu raia wa Burundi kuondoka nchini Kenya, akitaka suala hilo lichunguzwe kwa kina.
Kalasinga anasema inatia wasiwasi kuona mamia ya raia wa Burundi wakitafuta hati za kusafiria katika ubalozi wao jijini Nairobi, wakihofia kunyanyaswa au kufukuzwa nchini.
Mbunge huyo anataka serikali kubaini iwapo raia hao wanaondoka kwa hiari yao, ama wamekumbwa na vitisho, vitisho vya kufurushwa au aina nyingine ya unyanyasaji.
Kalasinga amesema Kenya imekuwa na historia ndefu ya kuwakaribisha watu kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika Mashariki, akisisitiza kuwa haki na heshima ya raia wa kigeni wanaoishi na kufanya kazi nchini kihalali lazima zilindwe.
Ametaka uchunguzi wa kina kufanywa ili kubaini chanzo cha kuondoka kwa raia hao wa Burundi, huku akisisitiza kuwa hakuna raia wa kigeni anayepaswa kulengwa kinyume cha sheria.
Wasiwasi huo unajiri huku serikali ikitoa muda wa siku tisini kwa raia wa mataifa ya Afrika Mashariki wasio na vibali halali kurekebisha hali yao ya uhamiaji, huku ikionya dhidi ya chuki dhidi ya wageni, unyanyasaji na kudhulumiwa.