Mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali imesababisha taharuki katika Shule ya Msingi ya Namamuka, eneo bunge la Kanduyi, Kaunti ya Bungoma, baada ya kung’oa paa la madarasa. Tukio hilo limewaacha mamia ya wanafunzi katika hali ya sintofahamu, huku shughuli za masomo zikiwa hatarini kuvurugika kutokana na uharibifu wa miundombinu. Uongozi wa shule sasa unaiomba serikali pamoja na wahisani kujitokeza na kusaidia katika ukarabati wa madarasa yaliyoathirika, ili kuhakikisha wanafunzi wanaendelea kujifunza katika mazingira salama. Akizungumza na waandishi wa habari, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Ruth Aswani, amesema shule imepata hasara kubwa kutokana na mvua hiyo, huku akieleza wasiwasi kuhusu usalama wa wanafunzi iwapo madarasa yaliyoharibiwa hayatakarabatiwa haraka.